NAIBU Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuuchunguza ujenzi wa kibanda cha kuhifadhia jenereta ya kuvuta maji katika mradi wa maji wa Ruaha Mbuyuni, wilayani Kilolo mkoani Iringa kinachodaiwa kujengwa kwa zaidi ya Sh Milioni 20. Aliyasema hayo juzi katika ziara yake ya siku moja wilayani humo kukagua miradi mbalimbali ya maji, ikiwemo ile inayosuasua kwasababu mbalimbali. “Nimepata taarifa eti kibanda hiki kimejengwa kwa zaidi ya Sh Milioni 20,” alisema na kuuliza ukweli wa taarifa hizo kwa mhandisi wa maji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Enock Basyagire aliyesema hakuwepo katika halmashauri hiyo wakati kikijengwa na kuomba akapitie nyaraka ili kujiridhisha. Aliwahimiza Takukuru kulifuatilia jambo hilo kwa haraka na kama kutakuwa na kile alichoita “matumizi mabaya ya fedha za umma” wahusika wakamatwe na kufikishwa mbele ya mkono wa sheria. Wakati huo huo, waziri Aweso ameoneshwa kusikitishwa kwake kuona katika mradi huo, tenki kubwa la kuhifadhi maji limejengwa katika eneo lisilo na chanzo cha maji; ambalo kwa mujibu wa taarifa ya mhandisi wa halmashauri hiyo, gharama yake ni zaidi ya Sh Milioni 45. “Huu ni uhuni, mmejenga tenki la Sh Milioni 45 na halijawahi kuwa na maji; mimi sio mtaalamu wa maji lakini najua, huwezi kujenga tenki katika eneo lisilo na chanzo cha uhakika cha maji, ni bora hapa mngechimba kisima kirefu huenda mngepata maji kwa ajili ya wananchi hawa wakati mkisubiri mradi mkubwa,” alisema. #kataarushwa #stopcorruption #dawasco #sdg #goal16 #takukuru https://www.instagram.com/p/Bt8g0yXhxf7/?utm_source=ig_tumblr_share&igshid=1ot57lvd3xcex










