Kila mtu anapenda kuheshimiwa. Lakini heshima haitolewi bila heshima. Yule anayependa kuheshimiwa, hana budi kugharamika heshima; kwani heshima haipatikani bure, ina gharama yake. Watu wanaweza kuheshimu tabia yako, akili yako, au uwezo wako wa kufanya kazi, lakini yapo mengine mengi yanayosababisha mtu aheshimiwe. Kwanza jitahidi kuwa mtu mwema. Siku zote kuwa mwema au mpole kwa kila mtu unayekutana naye, mchana au usiku, haijalishi kama ni mwenzi wako, watoto wako, wafanyakazi wenzako, wateja wako au mtu yeyote. Najua, ni rahisi kusema kuliko kutenda hasa unapokuwa umevurugwa. Lakini kama unapenda kuheshimiwa, wengine nao hupenda kuheshimiwa hivyohivyo. Wape wengine heshima hiyohiyo kama unayoitaka wewe. Tafuta njia au namna itakayokusaidia kusahau yale yaliyokuumiza, na kuwa mwema na mpole kwa watu. Mathalani: Mfungulie mwenzako mlango ofisini au popote, hata kama humjui, au jipange foleni unaposubiria huduma dukani au benki au popote pale. Tabasamu, na jifunze kusema tafadhali na asante inapowezekana. Pili, jiheshimu. Usiwe na tabia za dharau kama vile kununa pasi na sababu ya msingi, kurembua macho hasa kama wewe ni mwanamume, kutumia muda mwingi kwenye simu wakati ukiongea na mtu au watu, au kukatisha mazungumzo ya mtu unayeongea naye. Si tu kwamba tabia hizi ni dharau kwa yule unayeongea naye, bali huzuia hushiriki zaidi wa mazungumzo yenu au suluhisho la masuala mnayoyaongelea; na hutengeneza dosari inayoweza kuwa ya kudumu bila wewe mwenye dharau kujua. Kila mtu anayo haki ya kusikilizwa, hata kama siku zote hukubaliani na mawazo au maoni ya mtu fulani. Fikiria wewe ungependa kuheshimiwa vipi katika mazungumzo baina yako na mtu au watu, hasa mazungumzo ya maana, kisha uwaheshimu wengine hivyohivyo kama unavyopenda kuheshimiwa. Soma zaidi hapa: https://m.facebook.com/story.php?story_fbid=2668641119826366&id=100000415120038 #heshima #respect https://www.instagram.com/p/B1nrP5Bnji9/?igshid=fri5jvsm3rxj