MLINZI mkuu zamani wa Baba wa Taifa, Julius Nyerere, Peter Bwimbo (87) ameandika kitabu kwa mara ya kwanza akiweka wazi jinsi Mwalimu alivyotoroshwa kutoka katika mikono ya wanajeshi walioasi katika Maasi ya Jeshi ya mwaka 1964. Kitabu hicho: “ Peter D.M Bwimbo: Mlinzi Mkuu wa Mwalimu Nyerere” kimechapwa mwaka huu nchini na Kampuni ya Mkuki na Nyota na kina jumla ya kurasa 131 zinazoeleza mambo mbalimbali ambayo hayakuwahi kuelezwa waziwazi na yeyote. Kwa mfano, kitabu hicho; zaidi ya kueleza namna Nyerere alivyotoroshwa –kimeeleza pia namna aliyekuwa Waziri Mkuu, Rashidi Kawawa, alivyonusurika kufa kwa kuvuta hewa chafu nchini Misri kwenye miaka ya 1960 na namna Mwalimu pia alivyoamua kutopanda ndege iliyokuwa imeandaliwa na mwenyeji wake, aliyekuwa Rais wa Zaire, Mobutu Seseseko, kutokana na hofu za kiserikali. Ilivyokuwa wakati wa maasi Januari 20, mwaka 1964, askari wa Kiafrika waliokuwa ndani ya Jeshi la KAR waliasi kwa madai kwamba ingawa Tanganyika ilikuwa imepata Uhuru, bado jeshi hilo lilikuwa chini ya Waingereza na wanajeshi wengine wenye asili ya Kiasia. Katika kitabu hicho, Bwimbo ameandika kwamba maasi hayo yalitokea ghafla pasipo mipango hiyo kufahamika hata kwa Idara ya Kikachero ya wakati huo (Special Branch) na kwamba wahusika hawakufahamika mapema mpaka walichopanga kilipokamilika na hatimaye maasi kuanza. Ni maasi hayo ndiyo yaliyosababisha KAR kuvunjwa na hatimaye kuundwa kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) pamoja na Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) kama inavyofahamika sasa. Operesheni Magogoni Bwimbo anasema katika kitabu hicho kwamba aliipachika kazi ya kumwokoa Mwalimu na Kawawa wasitekwe na waasi waliokuwa wamevamia Ikulu jina la Operesheni Magogoni, kwa vile kivuko kilichotumika kuwaondoa viongozi hao kutoka Ikulu na kuwapeleka Kigamboni kilikuwa kinafahamika kwa jina la Magogoni. “ Nilipigiwa simu majira ya saa 8 usiku na ofisa wa kitengo chetu aliyekuwa mkuu wa zamu usiku huo hapo Ikulu, Leon Kazimili, kwamba kuna taarifa kuwa katika kambi ya Calito (Lugalo) palikuwa na dalili kuonyesha kuwa imevamiwa na majeshi ya kigeni usiku huo; Januari 20, 1964. “ Niliamka haraka kuelekea Ikulu nikiwa na gari langu kwa sab